Faith in God is not an Option

Blogger WidgetsJesus Loves You

Wednesday, 29 January 2014

Namna ya Kushinda Utumwa wa Dhambi


Somo:  Utumwa wa Hiyari na namna ya kushinda.

Fungu kuu: “ Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo”.Wagalatia 5:13

Katika Dunia ya leo kila nchi iko huru. Hata wananchi wanafurahia kwamba nchi zao ziko huru na kuna sherehe maalum za kusheherekea uhuru. Leo hatusikii tena habari ya Biashara ya utumwa. Kwa namna hali ilivyo tunaweza kwa haraka kusema Dunia iko huru, watu wako huru. Lakini hebu ngoja kidogo, Ni kweli tuko huru?

Kila jioni ninapopita njiani nakutana na watu walioko kwenye Bar wakinywa. Miili yao inawahitaji kufanya hivyo la sivyo ‘hawajisikii’ vizuri. Wakiwa hawana hela watakopa, lakini lazima wanywe kilevi. Je hawa wako huru? Hii inatupeleka kujadili, uhuru ni nini?

Kwa lugha rahisi uhuru ni kuwa bila kifungo, kufanya yale utayatakayo bila shuruti. Kuamua bila kusukumwa na nguvu kutoka nje. Tukiyajua haya sasa, twaweza kusema tuko huru? Tafakari

Leo ninaona wakristo walio katika utumwa. Utumwa walioamua wenyewe. Tena wanaulipia hata hela utumwa huo, wako utumwani kwa Hiyari.Utumwa wa Ngono, utumwa wa kuangalia picha za ngono, utumwa wa kufanya Masturbation, utumwa wa Hasira na chuki, utumwa wa kutosamehe, utumwa wa  woga na mashaka, utumwa wa umbeya na masengenyo. Utumwa, utumwa, utumwa. Ziko tabia zilizowashika wakristo na inakuwa vigumu kuziacha. Huu wote ni utumwa.

Lakini nina habari njema kwako! Bwana Yesu asifiwe kwamba si lazima hali iendelee kuwa hivyo. Inaweza kubadilika sasa, ndiyo, saa hii! Yuko Yesu mvunja utumwa. Yeye aliposimama mara ya kwanza katika sinagogi ili kutangaza kazi iliyomleta hapa duniani, aliomba apewe chuo cha nabii isaya, akatafuta mahali palipoandikwa juu ya kazi yake alipopata akasoma “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa” Luka 4:18. Kazi kuu ya Yesu ni kuvunja utumwa wa dhambi na kutuweka huru. Hatupaswi kuwa kwenye utumwa wa kitu chochote. Yesu anataka kutuweka huru! Wasikilizaji wakiwa bado  hawaelewi  vizuri akasema “Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu” Luka 4:21. Yaani aliwaambia, nimekuja kuwaweka huru!!  Leo pia maneno haya yanaweza kutimia masikioni mwako. Ndio, yanaweza kutimia masikioni mwako. Leo Yesu anaweza kuvunja laana za ukoo zinazokuandama. Baba alikuwa mzinzi na wewe umekuwa mzinzi. Dada alipata mimba nyumbani, na wewe unazalia nyumbani. Hizo ni laana na lazima zivunjike katika Jina la Yesu. Leo unaweza kuwa huru kutoka katika tabia ya kuangalia picha za ngono, leo Yesu anaweza kukuweka huru kutoka katika kila namna ya tabia mbaya na uraibu (addiction) uliyo nayo. Yote haya yanawezekana leo, maana hiyo ndiyo kazi ya Yesu –Kukuweka Huru.

Inawezekana umekata tamaa. Umeshawahi kujaribu kuacha lakini haikuwezekana. Au unaona umeshaingia sana kwenye hiyo tabia kiasi kwamba unaona huwezi kutoka. Je Yesu atashindwa kukutoa? Jibu ni Hapana. Hata iwe ni tabia gani na imekaa kwa muda mrefu kiasi gani, Yesu anaweza “Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka?  Naam, Bwana asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka; kwa maana nitateta na yeye atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu” Isaya 49:24 -25.

Wako wataalamu waliosomea kuwaondoa watu katika uraibu na kuwapa ushauri nasaha. Hawa nao wanaweza kukufanya uache tabia fulani kwa nje. Lakini hawawezi kukubadilisha kwa usahihi. Na pia hawawezi kukupa uzima wa milele. Ila Yesu ni zaidi. Biblia inapozungumzia uwezo wake wa kukuweka huru inasema ““Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli”. Yohana 8:36. Huru kweli kweli!! Jambo zuri kiasi gani!! Mimi sitaki tu kuwa huru, nataka kuwa Huru kweli kweli. Yesu anahitaji kukuweka huru, je uko tayari?  je utamwambia hapana? unawezaje kumwambia Hapana mtu aliyeacha enzi Mbinguni na kufa kwa ajili yako? Yeye ambaye kila siku anakuombea kwa Mungu na kuwatuma malaika zake wakulinde, je utamwambia Hapana? Mkubali Yesu leo, mpe yeye dhambi na tabia yako mbaya, naye ataibadilisha. Yko mtu anasema Hakuna anayenilazimisha kunywa Bia au kuzini ni mimi mwenyewe tu naamua, siku nikiamua kuacha naacha tu! Rafiki usijidanganye. Kama unaweza kuacha mwenyewe tu siku ukiamua, tafuta hiyo siku uamue tu mwenyewe uone kama hautarudi kuitafuta Bia au huyo mpenzi wako kesho yake. Hufanyi hayo mwenyewe, shetani ndio anakuendesha. Ila anakudanganya kwamba una uwezo wa kufanya na kuacha siku ukiamua. Shetani ni mwongo. Siku ukiamua, ataanzisha vita vikali vya kukurudisha. Njia pekee ni kumruhusu Yesu akubadilishe. Na usisubiri kesho, maana Kadri tabia mbaya inavyorudiwa inakuwa ngumu kuiacha. Usiongeze siku nyingine dhambini, Amua leo. Na yesu akikuweka huru, anakupa nguvu ya kutokurudia tena tabia hiyo

Mpendwa, Amua leo kuwa Huru. Mtwike Yesu dhambi yako, mwambie huwezi mwenyewe, unamtaka akusaidie. “Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu”. 1 Petro 5:7. Mungu akubariki. Na uniombee maana nitaanza mfufulizo wa mada za namna ya kutoka katika uraibu na dhambi za mazoea.

1 comments:

  1. Kama unabarikiwa na masomo haya. Tafadhali tupe comments zako, zinatutia sana moyo. Barikiwa

    ReplyDelete