Faith in God is not an Option

Blogger WidgetsJesus Loves You

Sunday, 2 February 2014

MAWASILIANO KATIKA NDOA




Moja ya mambo muhimu ya kuzingatia ili ndoa yako iwe bora ni Mawasilino. Wako wana ndoa ambao hawana uwezo wa kuzungumza pamoja kwa muda mrefu. Wao ni kusalimiana, kuulizana habari za chakula kiko wapi, kama mtoto amekula au la, na mambo Fulani machache ambayo hayaonyeshi kama ni wapenzi, ila tu ni watu wanaokaa nyumba moja. Hii si nzuri kwa ustawi wa Ndoa hiyo. Wengi walipokuwa wachumba kabla ya kuoana, walikuwa na vitu vingi vya kuzungumza pamoja. Walikuwa wanataniana na kucheka. Nini kimetokea sasa, kiasi kwamba ni kama hawana cha kuzungumza pamoja? Naomba niweke jambo moja sawa, kama hamna mazungumzo ya kutosha yasiyo na kanuni maalum, kama hamna uwezo wa kutaniana, kama hamzungumzi juu ya mapenzi yenu, ni wazi kwamba ndoa yenu hiyo ina shida kubwa!!

Wataalamu wanasema kwamba Moja ya tatizo kubwa katika ndoa ni hali ya wanandoa kutokuwa na mawasiliano au hali ya kusita katika kuanzisha mazungumzo. Wengi wa wanandoa wenye tatizo la mawasiliano wanajua kwamba hawazungumzi kama inavyotakiwa, lakini hawaelewi wafanyeje na wanaogopa kuanzisha mada hiyo kwa wenzi wao kwa kuogopa isije ikaleta ugomvi mwingine. Kwa namna hiyo tatizo linaendelea kuila ndoa  na wanandoa hao taratibu,mpaka hali inapokuwa mbaya zaidi na mmoja kushindwa kujizuia na kuamua kutoa yaliyo moyoni kwa hasira katika siku isiyo na jina.

Wataalamu wanasema ziko kanuni tatu(3) za msingi  ambazo ndio huonyesha kama mawasiliano katika ndoa hiyo yako vizuri au la,
  •  Kama wanandoa wanazingatia kanuni za kuzungumza na kusikiliza
  •  Kama wanandoa wanaweza kutatua matatizo yao katika namna bora iliyo ya kujenga
  •   Kama wanandoa wanapata muda mzuri kila siku wa kuzungumzia kwa pamoja juu ya hisia zao mbalimbali bila kusita au kuogopa kukosolewa


Kuna watu hawaelewi hata nini maana ya mawasiliano. Mawasiliano ni kuongea, kusikiliza na kuelewa kile kinachoongelewa. Ukisoma tu hapa, utaona ni rahisi sana. Lakini uhalisia unapokuja, ugumu wake ndio huonekana. Msingi mkubwa wa mazungumzo siyo katika kuongea tu, bali mazungumzo hujenga mahusiano. Hili ni muhimu kulifahamu, kwamba kama hamna mazungumzo mazuri na yafaayo, basi mahusiano yenu yataharibika.
Kuna mambo ambayo wana ndoa wamezoea kuyafanya, ambayo huwafanya wenzi wao wakwazike na kutojisikia kuendelea na mazungumzo. Mambo haya yanapaswa kuachwa mara moja.

1.       Utoaji wa lugha za Kuamrisha.
Maneno kama ‘Hebu njoo’, ‘Harakisha unanichelewesha’ au ‘usirudie tena’ na mengine kama hayo humfanya anayeambiwa asijisikie kama mwenzi bali aone amedharauliwa. Wako wanawake na wanaume wengi wanaofanya haya wengine kwa kujua au kwa kutokujua. Wanawake huweza kusema ‘ Usiwe unaacha socks zako sebuleni’ au ‘ukijisaidia haja ndogo uwe unamwamwaga maji,’  au ‘usitafune chakula hivyo’ n.k. maneno haya huonekana madogo kwa msemaji lakini kwa anayeambiwa yana madhara makubwa. Mwanaume hapendi maneno hayo kwa sababu yana amri ndani yake na yanamwonyesha kwamba hajui. Maneno hayo amekuwa akiambiwa na mama yake tangu utoto, ‘usifanye hivi…’ n.k. Kusikia mke wake naye anajifanya mama yake kwa kumuamrisha husababisha hasira. Na mara nyingi jibu litakalotoka hapo, halitakuwa zuri. Au mume ataaamua kuwa kimya tu asijibu chochote. Sasa hali itakuwa mbaya zaidi mke atakapouliza tena, ‘umenielewa lakini’? Hapo kitakachojibiwa, mke hatakaa asahau.
Wanawake kadhalika nao hawapendi amri. Na asili ya wanaume wengi wa kiafrika ni amri. Kwa hiyo hali ni mbaya. Kama kuna mahali wanandoa wamepanga kwenda, na wanawake kawaida yao huchukua muda mrefu mno kujiandaa, sasa wanaume wengi husema “Maliza haraka Bwana, unanichelewesha’ neno hilo linaweza likaharibu mood ya mkeo siku nzima, na sherehe yote itaingia nyongo. Wanawake wengi hawataki kuamrishwa na waume zao, wenyewe wana amini kwamba mume anapaswa awe mvumilivu kwake, mtu wa mapenzi, kwa hiyo ukiamrisha tu anakuona adui.

2.       Ukosoaji  na Kuhukumu wakati wa Mazungumzo
Kama liko jambo baya sana katika mazungumzo ni tabia ya kukosoa. Tena mbaya zaidi kumkosoa mwenzi wako mbele ya watu wengine. Wako baadhi ya wanawake ambao huwa ni ‘wajuaji’. Mume akisema jambo wao hujiandaa kumrekebisha. Mfano, Mume anasema ‘ Bwana john, sisi tutakusaidia kupata nafasi kwenye ile shule anayosoma mtoto wetu ni shule nzuri’ Mke anakosoa ‘utamsaidiaje wakati Yule mwalimu tunayemjua alishahama’,Mume ‘Ok, kumbe alishahama, lakini haina shida, wewe njoo jumatatu mimi nitakupeleka na tutaongea na……..’ Mke anaingilia ‘ Jumatatu si ndio tulipanga tukaangalie kile kiwanja, sasa utampelekaje’. Mfano huu unaonesha mwenzi mmoja anayeonekana anajua sana. Mambo anayoyasema ni kweli, lakini hampi nafasi mwingine kumalizia maongezi. Na anamkosoa mbele ya mtu mwingine na kumfanya aonekane mjinga. Hii si nzuri.
Wako pia wanaohukumu. Hawa ni wale ambao hawasikilizi mpaka mwisho lakini wanajifanya wameshaelewa ulichotaka kusema. Mfano mke anamwambia mume ‘ Kuna gauni nimeliona kwenye Boutique mjini ni zuri sana….’ Mume anahukumu ‘ hatuna hela kwa sasa, yako mambo mengi ya kufanya siyo kuvaa vaa tu kila siku’. Huku ni kuhukumu. Mke hakusema anataka kununua, lakini mume ameshahukumu. Yaweza kuwa mke alikuwa anasema hivyo, ili akupe wazo la kuanzisha Boutique yenye nguo nzuri kama ile, au alikuwa anakupa wazo la kumnunulia mama yako nguo hiyo kama zawadi. Lakini hayo yote hutaelewa tena, maana mke umeshamuudhi na hataweza kuendelea kuongea, angalau kwa muda huo.

3.       Kunyamaza Kimya
Ukimya nao hutumika na wana ndoa kama silaha ya ‘kuumizana’ mioyo. Wanaume na wanawake hutumia silaha hii, ila kwa njia tofauti. Ukiona mwanaume amenyamaza kimya, hataki kuzungumza, ujue Hisia za Hasira au woga huwa zinatengenezeka ndani. Mwanamke huwa anatumia silaha ya kunyamaza kimya kama kulipiza kisasi kwa aina Fulani ya ‘uonevu’ aliofanyiwa na mume wake. Wako wanawake waliofundishwa kuvumilia, na kwa hiyo wao bora wanyamaze kimya, ingawa wanaumia ndani kuliko kuzungumzia hayo. Na wako wanaume ambao wana amini kwamba kueleza hisia zako kwa mke wako, ni kutokuwa mwanaume halisi, bali ni kuonyesha hali ya kike. Kwa hiyo hawa wakipatwa na matatizo kazini au njiani, watabaki kimya na hasira zao mpaka ziishe zenyewe lakini hawatawaeleza wake zao wanavyojisikia kwa sababu kufanya hivyo siyo uanaume kamili. Kunyamaza Kimya si jambo zuri! Ndoa inapaswa iwe na mazungumzo.

Tutaendelea na mada hii……..