Somo: Utumwa wa Hiyari na namna ya kushinda.
Fungu kuu: “ Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu
usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo”.Wagalatia 5:13
Katika Dunia ya leo kila nchi iko huru. Hata wananchi wanafurahia kwamba nchi
zao ziko huru na kuna sherehe maalum za kusheherekea uhuru. Leo hatusikii tena
habari ya Biashara ya utumwa. Kwa namna hali ilivyo tunaweza kwa haraka kusema
Dunia iko huru, watu wako huru. Lakini hebu ngoja kidogo, Ni kweli tuko huru?
Kila jioni ninapopita njiani nakutana na watu walioko kwenye Bar wakinywa.
Miili yao inawahitaji kufanya hivyo la sivyo ‘hawajisikii’ vizuri. Wakiwa
hawana hela watakopa, lakini lazima wanywe kilevi. Je hawa wako huru? Hii
inatupeleka kujadili, uhuru ni nini?
Kwa lugha rahisi uhuru ni kuwa bila kifungo, kufanya yale utayatakayo bila
shuruti. Kuamua bila kusukumwa na nguvu kutoka nje. Tukiyajua haya sasa,
twaweza kusema tuko huru? Tafakari
Leo ninaona wakristo walio katika utumwa. Utumwa walioamua wenyewe. Tena
wanaulipia hata hela utumwa huo, wako utumwani kwa Hiyari.Utumwa wa Ngono,
utumwa wa kuangalia picha za ngono, utumwa wa kufanya Masturbation, utumwa wa
Hasira na chuki, utumwa wa kutosamehe, utumwa wa woga na mashaka, utumwa wa umbeya na
masengenyo. Utumwa, utumwa, utumwa. Ziko tabia zilizowashika wakristo na
inakuwa vigumu kuziacha. Huu wote ni utumwa.
Lakini nina habari njema kwako! Bwana Yesu asifiwe kwamba si lazima hali
iendelee kuwa hivyo. Inaweza kubadilika sasa, ndiyo, saa hii! Yuko Yesu mvunja
utumwa. Yeye aliposimama mara ya kwanza katika sinagogi ili kutangaza kazi
iliyomleta hapa duniani, aliomba apewe chuo cha nabii isaya, akatafuta mahali
palipoandikwa juu ya kazi yake alipopata akasoma “Roho wa Bwana yu juu yangu,
Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa” Luka 4:18. Kazi kuu ya Yesu ni kuvunja utumwa wa dhambi na
kutuweka huru. Hatupaswi kuwa kwenye utumwa wa kitu chochote. Yesu anataka
kutuweka huru! Wasikilizaji wakiwa bado hawaelewi vizuri akasema “Akaanza kuwaambia, Leo
maandiko haya yametimia masikioni mwenu” Luka 4:21. Yaani aliwaambia, nimekuja
kuwaweka huru!! Leo pia maneno haya
yanaweza kutimia masikioni mwako. Ndio, yanaweza kutimia masikioni mwako. Leo
Yesu anaweza kuvunja laana za ukoo zinazokuandama. Baba alikuwa mzinzi na wewe
umekuwa mzinzi. Dada alipata mimba nyumbani, na wewe unazalia nyumbani. Hizo ni
laana na lazima zivunjike katika Jina la Yesu. Leo unaweza kuwa huru kutoka
katika tabia ya kuangalia picha za ngono, leo Yesu anaweza kukuweka huru kutoka
katika kila namna ya tabia mbaya na uraibu (addiction) uliyo nayo. Yote haya
yanawezekana leo, maana hiyo ndiyo kazi ya Yesu –Kukuweka Huru.
Inawezekana umekata tamaa. Umeshawahi kujaribu kuacha lakini haikuwezekana.
Au unaona umeshaingia sana kwenye hiyo tabia kiasi kwamba unaona huwezi kutoka.
Je Yesu atashindwa kukutoa? Jibu ni Hapana. Hata iwe ni tabia gani na imekaa
kwa muda mrefu kiasi gani, Yesu anaweza “Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa
mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka? Naam, Bwana
asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi
mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka; kwa maana nitateta na yeye
atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu” Isaya 49:24 -25.
Wako wataalamu waliosomea kuwaondoa watu katika uraibu na kuwapa ushauri
nasaha. Hawa nao wanaweza kukufanya uache tabia fulani kwa nje. Lakini hawawezi
kukubadilisha kwa usahihi. Na pia hawawezi kukupa uzima wa milele. Ila Yesu ni
zaidi. Biblia inapozungumzia uwezo wake wa kukuweka huru inasema ““Basi Mwana
akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli”. Yohana 8:36. Huru kweli kweli!!
Jambo zuri kiasi gani!! Mimi sitaki tu kuwa huru, nataka kuwa Huru kweli kweli.
Yesu anahitaji kukuweka huru, je uko tayari? je utamwambia hapana? unawezaje kumwambia
Hapana mtu aliyeacha enzi Mbinguni na kufa kwa ajili yako? Yeye ambaye kila
siku anakuombea kwa Mungu na kuwatuma malaika zake wakulinde, je utamwambia
Hapana? Mkubali Yesu leo, mpe yeye dhambi na tabia yako mbaya, naye
ataibadilisha. Yko mtu anasema Hakuna anayenilazimisha kunywa Bia au kuzini ni
mimi mwenyewe tu naamua, siku nikiamua kuacha naacha tu! Rafiki usijidanganye.
Kama unaweza kuacha mwenyewe tu siku ukiamua, tafuta hiyo siku uamue tu
mwenyewe uone kama hautarudi kuitafuta Bia au huyo mpenzi wako kesho yake.
Hufanyi hayo mwenyewe, shetani ndio anakuendesha. Ila anakudanganya kwamba una
uwezo wa kufanya na kuacha siku ukiamua. Shetani ni mwongo. Siku ukiamua,
ataanzisha vita vikali vya kukurudisha. Njia pekee ni kumruhusu Yesu
akubadilishe. Na usisubiri kesho, maana Kadri tabia mbaya inavyorudiwa inakuwa
ngumu kuiacha. Usiongeze siku nyingine dhambini, Amua leo. Na yesu akikuweka
huru, anakupa nguvu ya kutokurudia tena tabia hiyo
Mpendwa, Amua leo kuwa Huru. Mtwike Yesu dhambi yako, mwambie huwezi
mwenyewe, unamtaka akusaidie. “Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana
yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu”. 1 Petro 5:7. Mungu akubariki. Na
uniombee maana nitaanza mfufulizo wa mada za namna ya kutoka katika uraibu na
dhambi za mazoea.